Blog Entry

Sunday, August 30, 2009

JOYCE KIRIA AFYATUKA


Akipasha kisawasawa, Joyce ambaye huendesha kipindi cha Bongo Movies kila siku ya Jumatano, alisema kuwa, kuibwa kwa kazi za wasanii kila kukicha kwa namna moja au nyingine kunachangiwa na COSOTA kutokuwa na ubunifu mpya katika kupanga mikakati ya kuhakikisha tabia hiyo inakoma mara moja.

Alisema kuwa, wasanii wamekuwa wakipigania maisha yao kuwa bora kupitia sanaa yao, “lakini wezi wanawaangusha na COSOTA kila siku wamekuwa wakituambia wamekamata wezi wa kazi za wasanii, lakini hawajawahi kusema watawafanya nini baada ya hapo,” alisema Joyce.

Joyce alionekana kuwa mbogo katika suala hilo baada ya kurusha maneno makali zaidi kwa COSOTA na kudai kuwa, wamekuwa wakiwafumbia macho wezi wa kazi hizo hali inayozua maswali kibao yenye majibu kiduchu.

Aliendelea kupasha kwamba, kilichomsukuma kutoboa ukweli huo ni baada ya COSOTA kuitisha mkutano na Mapaparazi siku ya Jumatatu pale MAELEZO na kuelezea fahari yao kwa kukamata Kompyuta na kazi feki za wasanii wa Bongo.

Akahoji: “Lakini baada ya pale Mkinga (Mtendaji Mkuu wa COSOTA) hakusema hao waliokamatwa watafanywa nini, ingekuwa ni wauza madawa ya kulevya wale unadhani nini kingetokea?”

Aidha, Joyce aliendelea kuweka wazi kwamba, katika kikao hicho, alijikuta akibaki peke yake baada ya waandishi kuonesha dalili za kutomuunga mkono kwa yeye “kuisimanga” COSOTA hali iliyosababisha kutokea kwa zomeazomea dhidi yake.

Akasema baada ya hapo, siku ya Jumapili aliamua kurekodi kipindi cha Bongo Movies kwenye Ukumbi wa New World Cinema, Mwenge jijini Dar na kuwaalika wasanii wa Bongo na watendaji wakuu wa COSOTA ili kujadili nini cha kufanya kufuatia wizi wa kila kukicha wa kazi za wasanii.

Akasema: “Matokeo yake, Mkinga hakutokea na wala hakutoa sababu, nilipompigia simu akawa hapokei, ndiyo maana ukaona wasanii wakainanga sana COSOTA, maana waliona kama wanafanyiwa usanii tu.”

Hata hivyo, Joyce alisema baada ya kikao cha wasanii hao, Mkinga alimpigia simu na kumwambia alishindwa kufika na hakupokea simu kwa sababu alikuwa kwenye kikao.

Katika kikao hicho, wasanii waliishambulia Serikali na COSOTA yake kwamba, haina habari katika kuwalinda wasanii nchini huku wakitoa kipaumbele kwenye nyanja nyingine ambazo hazina tija sana kwa pato la Serikali.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, msanii Hissan Muya “Tino” alifikia mahali akasema wasanii wapewe vibali vya kuyateketeza maduka yatakayobainika kuuza kazi feki za wasanii wa Bongo.

Wasanii walioivurumishia hasira zao Serikali ni pamoja na Suzane Lewis “Natasha”, Single Mtambalike “Richi,” Jacob Steven “JB”, Hissan Muya “Tino”, John Lister (Prodyuza), Kulwa Kikumba “Dude” na wengine ambao walifika.

No comments:

Post a Comment